Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi imeanza Rasmi kutekeleza Mpango kabambe wa Kampeni ya Chanjo na Utambuzi wa Mifugo Kitaifa, ambapo leo imetoa chanjo kwa mifugo takribani 400 ili kuboresha na kuleta mabadiliko makubwa katika Sekta ya Mifugo na kuondoa vikwazo ambavyo vimekuwa vikizuia Mifugo na mazao yake kuuzwa katika nchi zenye Masoko mazuri.Akizungumza katika zoezi la Uhamasishaji na Utoaji Chanjo za Mifugo leo Julai 3, 2025 Wilayani Babati Mkoani Manyara, Mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya ya Babati ambaye ndiye alikuwa Mgeni Rasmi wa zoezi la Uhamasishaji na Utoaji wa Chanjo za Mifugo Wilayani hapo, na Katibu Tawala Wilaya ya Babati, Ndg. Thobias Abwaro amesema zoezi la Utoaji Chanjo na Utambuzi wa Mifugo ni zoezi endelevu ambalo ni la muda mrefu na litaleta tija kwa wafugaji na Taifa zima kwa ujumla.“Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ameridhia kugharamia Mpango wa Utoaji chanjo na Utambuzi wa Mifugo kwa miaka 5 kutoka 2025 hadi 2029, ambao utagharimu kiasi cha shilingi Bilioni 216 za Kitanzania, na ametoa ruzuku ya asilimia mia Moja kwa chanjo za kuku ambayo ni sawa na bure, na asilimia 50% kwa chanjo za ng'ombe na mbuzi/kondoo, ambapo ng'ombe ni tshs. 500/= na mbuzi/kondoo ni tshs. 300/=, hii yote ni kuonesha ni jinsi gani anajali Mifugo na Wafugaji.” ameseama Ndg. Abwaro Aidha, Ndg. Abwaro amesema kwa muda mrefu uchanjaji wa Mifugo umekuwa ukifanyika kidogo kidogo katika ngazi za Mamlaka ya Serikali za Mitaa, mashamba makubwa na wafugaji mmoja mmoja bila kuwa na uratibu wa pamoja ambao hauwezi kutokomeza Magonjwa hayo ya Mifugo, kwani ili kutokomeza Magonjwa hayo inabidi kuchanja Mifugo angalau kwa asilimia 70%.Vilevile, Ndg. Abwaro kwa niaba ya wafugaji wa Mkoa wa Manyara amemshukuru Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuridhia na kutoa Ruzuku ya Kampeni ya Chanjo za Mifugo ambayo inaenda kuwanufaisha wafugaji na kuwaletea tija Kibiashara.
Naye, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI), Prof. Erick Komba, amesema kuwa Mifugo inaathiriwa sana na magonjwa mbalimbali ambayo yanapelekea vifo vya Mifugo na mazao yake kutokuwa bora na hata kupelekea kutokidhi viwango vya Masoko ya nje."Ndio maana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan ameridhia na kuiwezesha Sekta hii ili kuboresha maisha ya Mifugo na wafugaji, na kutanua wigo wa Masoko ya nje" amesema Prof. KombaPia, Prof. Komba amesema kuwa ni Imani yake kuwa zoezi hili litafanikiwa kwa asilimia mia Moja na chanjo hizi zitasaidia kuimarisha Mifugo na hatimae kuwa na mazao Bora zaidi.Halikadhalika, Prof. Komba amewataka wafugaji kujitokeza kwa wingi katika kuchanja Mifugo yao ili kutokomeza Magonjwa hayo ya Mifugo kwani Kampeni hii ni fursa adhimu kwa wafugaji.
Halmashauri ya wilaya ya Babati
Anwani: P.O BOX 400, Babati.
Simu ya mezani: Simu Na. 027-2531011
Simu ya Kiganjani: 0620444641,075486577
Barua pepe: info@babatidc.go.tz,ded@babatidc.go.tz
Copyright ©2020 Babati District Council . All rights reserved.