IDARA YA MAJI
Huduma ya maji katika Halmashauri ya Wilaya ya Babati hadi kufikia Februari 2017 inatolewa kwa watu wapatao 224,922 ambao ni sawa na asilimia 62.7 ya wakazi wote.
HALI YA MIRADI YA MAJI WILAYANI
Huduma ya maji safi katika Halmashauri ya Wilaya ya Babati hutolewa kwa njia zifuatazo:-
1. Miradi ya maji ya Mtiririko – 42
2. Miradi ya maji ya visima virefu – 8
3. Miradi ya maji visima vifupi – 144
4. Miradi ya maji ya mabwawa – 13
5. Malambo yapo – 6
6. Miradi ya uvunaji wa maji ya mvua - 43
MAJUKUMU YA IDARA
Idara ya Maji ikiwa ni moja ya Idara chini ya Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Wilaya inajishughulisha na kumsaidia/kumshauri Mkurugenzi Mtendaji Wilaya katika mambo yafuatayo:-
Kuandaa mipango na bajeti ya utoaji wa huduma ya maji kwa wananchi kwa mwaka.
Kuratibu shughuli za huduma ya maji wilayani.
Kusimamia ujenzi wa miundombinu na ukarabati wake wilayani.
Kutoa elimu na kuhamasisha wananchi juu ya usimamizi na uendeshaji wa miradi ya maji kwa maendeleo endelevu kwa kushirikiana na idara zingine.
Kuandaa taarifa na takwimu za huduma ya maji na kuziboresha kila wakati.
Mengineyo yanayojitokeza na kupangiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya.
MAFANIKIO
Kwa kuitikia utekelezaji wa sera ya maji ya mwaka 2002 na sheria ya maji na usafi wa mazingira No. 12 ya mwaka 2009, Jamii imeanzisha jumla ya vyombo vya watumia maji 13 (8 vimesajiliwa, 2 vipo katika hatua ya uundwaji na 3 katika hatua ya usajili), vilevile kuna mifuko ya maji 39 ya kijiji. Idara kwa kushirikiana na mashirika yasiyo ya kiserikali inaendelea kuhamasisha jamii uanzishaji wa vyombo vya watumiaji maji kisheria pamoja na uboreshaji wa vyombo hivyo. Pia Halmashauri ina jumla ya Mamlaka za maji za miji midogo 4 ambazo ni Magugu, Gallapo, Dareda na Bashnet.
Baada ya jamii kutambua umuhimu wao katika utekelezaji wa miradi ya maji vijijini, Taasisi mbalimbali ambazo ni WaterAid, World Vision, Fide, FACFna Dorcas zinashiriki katika ujenzi wa miradi mbalimbali ya maji pamoja na kuhamasisha jamii kuanzisha vyombo vya kijamii vya kusimamia uendeshaji na matengenezo ya miradi ya maji katika Halmashauri yetu
CHANGAMOTO
Uelewa mdogo wa wananchi katika masuala ya usimamizi wa rasilimali za maji. Jamii kutojali muda wa utekelezaji wa miradi kwa kuchelewesha kuchangia/ kutoa nguvu kazi na kusababisha kuongezeka kwa gharama za ujenzi wa miradi.
Uharibifu na uchafuzi wa vyanzo vya maji kama vile, kukata miti, kulishia mifugo na kulima kwenye vyanzo vya maji.
Kupungua kwa maji kwenye vyanzo vya maji vinavyotumika kutokana na mabadiliko ya tabia nchi hususani katika kipindi cha kiangazi.
Uchakavu wa miundombinu ya miradi kutokana na kujengwa muda mrefu uliopita na kukosa fedha za kutosha za ukarabati.
Vyombo vya watumia maji bado ni vichache na bado vina udhaifu wa uongozi.
Kutokuwepo na fedha za kutosha kwa ajili ya kazi za dharura, kama vile kuharibika kwa pampu na bomba kupasuka.
Ukosefu wa vitendea kazi kwa ajili ya Wataalamu wakati wa ukarabati/ujenzi wa miradi (Kama Pikipiki)
MIKAKATI
Kuwezesha jamii kuwepo kwa vyombo madhubuti vya watumia maji, vilivyoimarika vitakavyosimamia uendeshaji na matengenezo ya miradi ya maji.
Kuelekeza nguvu (fedha) katika miradi michache itakayokamilika mapema badala ya kuwa na msururu wa miradi isiyokamilika.
Kuimarisha usimamizi wa rasilimali za maji na hifadhi ya vyanzo vya maji kwa kuiwezesha jamii kuanzisha vyombo vya kusimamia vizuri matumizi ya maji pamoja na hifadhi ya vyanzo vya maji.
Kutengeneza mazingira mazuri zaidi ya sekta binafsi kushiriki katika ujenzi, uendeshaji na matengenezo ya miradi ya maji.
Kuhamasisha jamii kujenga miundombinu ya kuvuna maji ya mvua na kutumia maji yaliyoko chini ya ardhi kwa kuchimba visima.
Kuhakikisha huduma ya maji inaongezeka kutoka 62.7% iliyopo mpaka kufikia 90 ifikapo Desemba, 2020.
Halmashauri ya wilaya ya Babati
Anwani: P.O BOX 400, Babati.
Simu ya mezani: Simu Na. 027-2531011
Simu ya Kiganjani: 0620444641,075486577
Barua pepe: info@babatidc.go.tz,ded@babatidc.go.tz
Copyright ©2020 Babati District Council . All rights reserved.