*Mwananchi wa Manyara kupata Maji safi na salama ni haki yako ya msingi – RC Sendiga.Mkuu wa Mkoa wa Manyara Mhe. Queen Cuthbert Sendiga, amewaambia wananchi wa kijiji cha Gidabaghar kilichopo Halmashauri ya Wilaya ya Babati Mkoani humo kuwa kupata maji safi na salama ni haki yao ya msingi na sio suala la kuomba na kunyenyekea.
RC Sendiga ameyasema hayo Machi 21, 2024 akiwa kwenye mkutano wa hadhara katika Kijiji hicho ikiwa ni muendelezo wa ziara yake ya kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo katika sekta ya Afya na Maji. Akizindua mradi wa maji wa Gidabaghar uliodhaminiwa na kujengwa na shirika la World Vision kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Babati chini ya RUWASA Wilaya ya Babati, amesema Mradi huo wenye thamani ya Shilingi 291,669,700 unatarajiwa kuhudumia zaidi ya Wananchi 1,500.
Pia RC Sendiga ametembelea na kukagua Mradi wa Maji wa Boay ambao upo kwenye kipindi cha mwaka mmoja wa matazamio na kubaini changamoto kadhaa na kuwaagiza wasimamizi wa Chombo kuongea na Wananchi na kuwasikiliza ili waweze kutatua changamoto za mradi huo pamoja RUSAWA kuongeza vituo vya umma vya kuchotea maji (DP) nyingine katika kijiji hicho ili kutanua mtandao wa Maji na kuwafikia wananchi wengi zaidi.
Sambamba na hilo RC Sendiga ametembelea na kukagua Zahanati ya Kijiji cha Boay na kusisitiza suala la msawazo wa Watumishi ili kuleta usawa wa uhitaji wa watumishi katika Zahanati husika ili kusaidia kutoa huduma bora na kwa wakati, pamoja na kutoa maagizo kwa Mkuu wa Wilaya ya Babati, Wataalamu na viongozi wa kijiji hicho kuitisha kikao kwajili ya kusikiliza na kutatua kero za wananchi jumatatu ya tarehe 25 Machi 2024.
Halmashauri ya wilaya ya Babati
Anwani: P.O BOX 400, Babati.
Simu ya mezani: Simu Na. 027-2531011
Simu ya Kiganjani: 0620444641,075486577
Barua pepe: info@babatidc.go.tz,ded@babatidc.go.tz
Copyright ©2020 Babati District Council . All rights reserved.