Mkuu wa Wilaya ya Babati, Mhe. Emmanuela Mtatifikolo Kaganda, leo tarehe 09 Julai 2025 ameweka jiwe la msingi katika Mradi wa ujenzi wa boksi kalavati kwenye Barabara ya Mamire-Qash, unaotekelezwa kwa lengo la kuimarisha miundombinu ya mawasiliano kati ya kata tatu muhimu: Galapo, Mamire na Endakiso.Katika tukio hilo, Mhe. Kaganda amewataka wananchi, hususan vijana, kuwa walinzi wa mali za Serikali na kuhakikisha hakuna uharibifu unaofanyika katika eneo la daraja hilo, kwani ni sehemu ya uwekezaji mkubwa wa Serikali kwa ajili ya wananchi. Alisisitiza kuwa uzalendo unaanza kwa kulinda miradi inayotekelezwa ili iweze kudumu na kutumika kwa manufaa ya muda mrefu.
Mwenyekiti wa Kijiji husika amepongeza Serikali kwa mradi huo na kusema kuwa daraja hilo litakuwa kiunganishi muhimu kwa wakazi wa kata hizo, hasa wakati wa mvua ambapo eneo hilo lilikuwa likisababisha changamoto kubwa za usafiri na usafirishaji wa mazao.Wananchi waliohudhuria hafla hiyo wameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa kusikia kilio chao na kufanikisha ujenzi wa daraja hilo, wakikiri kuwa litakuwa msaada mkubwa sana katika shughuli zao za kila siku na kuinua uchumi wa maeneo hayo.
Daraja hilo linatarajiwa kuzinduliwa rasmi na Mbio za Mwenge wa Uhuru 2025 tarehe 15 Julai, wakati Mwenge utakapo kimbizwa katika miradi ya Maendeleo katika Halmashauri ya Wilaya ya Babati, ikiwa ni ishara ya kuthamini na kutangaza mafanikio ya Serikali katika kuleta maendeleo ya kweli kwa wananchi.
Halmashauri ya wilaya ya Babati
Anwani: P.O BOX 400, Babati.
Simu ya mezani: Simu Na. 027-2531011
Simu ya Kiganjani: 0620444641,075486577
Barua pepe: info@babatidc.go.tz,ded@babatidc.go.tz
Copyright ©2020 Babati District Council . All rights reserved.