Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Babati Vijijini, Mhe. Daniel Sillo, amezindua bweni la Wasichana katika Shule ya Sekondari Qash, lililojengwa kwa msaada wa Shirika la So They Can Tanzania kwa gharama ya shilingi milioni 187. Bweni hilo lenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 80 limejengwa kwa ushirikiano na wananchi ambao walichangia asilimia 7 ya gharama za ujenzi huo.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, leo Mei 10, 2025 katika Shule ya Secondary Qash iliyopo wilayani Babati Mhe. Sillo amewashukuru wananchi kwa mapokezi mazito na kujitolea katika kuchangia maendeleo ya elimu.
Mhe. Sillo ameipongeza Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi mahiri wa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuweka mazingira wezeshi kwa wawekezaji kwa kuendelea kudumisha amani na usalama nchini.
Amesema kuwa, kutokana na jitihada hizo, Shirika la So They Can pamoja na wawekezaji wengine wameweza kuwekeza Tanzania katika miradi mbalimbali kwa utulivu na amani
Mbali na uzinduzi wa bweni hilo, Mhe. Sillo alieleza kuwa Serikali imeshaipatia halmashauri ya Wilaya ya Babati kiasi cha shilingi milioni 520 kwa aajili ya ujenzi wa mabweni manne katika Shule za Secondary Kisangaji na Gidas. Amesisitiza kuwa uwekezaji huo ni sehemu ya mkakati wa Serikali katika kuhakikisha inaboresha sekta ya elimu na ustawi wa wanafunzi.
Pamoja na hayo, Mhe. Sillo alitoa wito kwa viongozi wa dini na wananchi kuendelea kuliombea taifa kwa ajili ya kudumisha amani na utulivu, hasa katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi. Pia alitoa wito kwa wazazi, walezi, na viongozi kushiriki kikamilifu katika kupambana na ukatili wa kijinsia kwa kutoa taarifa pale wanapohisi vitendo vya kikatili vinafanyika, ili kuwalinda watoto na familia dhidi ya vitendo hivyo.
Halmashauri ya wilaya ya Babati
Anwani: P.O BOX 400, Babati.
Simu ya mezani: Simu Na. 027-2531011
Simu ya Kiganjani: 0620444641,075486577
Barua pepe: info@babatidc.go.tz,ded@babatidc.go.tz
Copyright ©2020 Babati District Council . All rights reserved.